
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mustapha Sabodo (pichani), amevitaka vyama vya upinzani nchini kuungana ili kuking’oa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani. Amesema iwapo Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vitaunganisha nguvu pamoja kwa kumsimamisha mgombea urais mmoja katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kazi ya kuing’oa CCM madarakani itakuwa rahisi.
Akizungumza jana katika Mkutano Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, uliofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, alikoalikwa kuhudhuria shughuli za ufunguzi, Sabodo alisema hivi sasa CCM kuna makundi yanayokigawa vipande vipande na kuhatarisha uimara wake.
Alisema kwa sababu ya hali ilivyo ndani ya CCM, Rais Jakaya Kikwete akiulizwa leo nani atamrithi kwenye wadhifa alionao sasa wa urais, itakuwa ni changamoto kwake, tofauti na kipindi cha Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alijua kuwa anayemfuatia ni Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia alijua mrithi wake ni nani.
Sabodo, ambaye alizungumza kwa niaba ya wageni waalikwa katika mkutano huo, alitangulia kutoa maneno ya kujigamba kuwa anazo fedha za kutosha, kabla ya kutoa mchango wa Sh milioni 20 kwa ajili ya kuendeshea shughuli za uchaguzi huo na kuahidi kuchangia ujenzi wa visima vya maji kwa kila Jimbo la Mbunge wa chama hicho.
“Mimi nina hela, kuna bahasha ndogo nakupongeza… vyama vya siasa ili kuing’oa CCM madarakani mfanye kazi kubwa kwa kushirikiana, msimamishe mgombea mmoja na kuepuka migogoro,” alisema Sabodo.
Awali katika hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema katika mchakato wa Katiba Mpya kuna haja ya kuwepo maridhiano ya kitaifa, kwa kutanguliza maslahi ya nchi na vyama yaje baadaye.
Akizungumzia kuuawa kwa Dk. Sengondo Mvungi pamoja na mashambulizi mengine yaliyowahi kutokea ya aina kama hiyo, Mbatia alisema kuna haja ya watawala kufuatilia na kutoa majibu ili kuepuka kuja kuulizwa hapo baadaye kama ilivyotokea nchini Kenya.
“Nchi hii ni yetu sote, tukiingia madarakani CCM msiogope mtakuwa salama. Watawala wafahamu kuwa kuna leo kuwepo madarakani na kesho wakaondoka, hawawezi kukimbilia kokote, nchi yetu ndiyo hii,” alisema Mbatia.
Alisema hata katika uchaguzi huo, wapiga kura wanapaswa kuzingatia uwezo wa mtu, uzalendo, kuwajibika, udugu, amani, utaifa na kwamba isifikie hatua ya kuchaguana kwa udini ndani ya chama.
Alitaja sifa za uongozi kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuongoza, mcha Mungu, mkweli na mwenye kuchukia uovu.
Katika nyanja ya elimu, Mbatia alisisitiza kauli yake aliyopata kuitoa bungeni kuwa nchi haina mtaala wa elimu na kinachofanyika sasa ni kung’atang’ata meno.
“Ukiingiza ufisadi kwenye elimu unaiua na matokeo yanatokana na uchumi mbovu katika elimu, kipindi nikiwa darasa la tano tulikuwa tunaimba wimbo mmoja wa msingi wa ujamaa, Mwalimu alitengeneza taifa la kijamaa, viongozi hawashushwi kutoka mbinguni, bali wanatengenezwa, leo hii tuko wapi,” alisema Mbatia.
Alisema kitabu cha somo la Civics cha darasa la sita kina nembo zinazopotosha uhalisia wa nembo ya Muungano.
Katika utalii, Mbatia alisema nchi ina vivutio vya utalii, lakini ni maskini, na kwamba kinachofanyika ni kupita kuombaomba, jambo ambalo linasababisha kupandikiza kwenye akili za watoto kuitwa akili za kuomba na kuitwa kupe.
Alisema Tanzania ni nchi ya pili kwa utalii duniani, lakini bado ni maskini, tofauti na Mauritius ambayo ina vivutio vya utalii 53 na ina nafasi ya vivutio 131, Uganda ina 29 na wameshika nafasi ya 105.
Pamoja na hilo, alisema kuna umaskini wa fikra ambao ni majungu, fitina, umbea, kusema uongo, chuki pamoja na uvivu wa kufikiri.
“Ukiwekeza vyema kwenye utalii na kuwapa uwezo wawekezaji wa ndani kama kina Sabodo, watajenga humu humu ndani, kwa nini kina Mengi, Bakhresa wasipewe uwezo nchi iweze kusonga mbele?” alihoji Mbatia.
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alisema chama hicho kitashinda kama kitazingatia misingi ya amani na utaifa kwa kuuweka mbele.
“Nawaasa wanachama wa NCCR-Mageuzi kuonyesha Watanzania kuwa si watu wa kusema tu, bila kutekeleza, ni mtihani kwenu kuhakikisha mnachagua viongozi bora wenye ukomavu na ustaarabu wa maono ya siasa kuwa ndio watawasaidia kama chama kuvuka katika migogoro na si kuuwa chama,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema chama hakiwezi kuongozwa kwa sheria pasipo busara, ukomavu wa kisiasa na kwa kuzingatia kanuni na kwamba kikifanikiwa kupata viongozi hao, kinaweza kujinadi kuchukua dola.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani vilivyofika mahali hapo, isipokuwa CCM ambacho kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Philip Mangula, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema vyama vya upinzani visiombeane ubaya kuwa kimoja kife, kwani hata kama kikiingia chama hicho madarakani na kuchukua viti vingi vya ubunge, bado demokrasia itakuwa shakani, kwani haijaimarika.
Mbowe aliiomba Ofisi ya Msajili isiwajengee ukondoo wa utiifu, bali ihakikishe inatenda haki na pia NCCR kuimarika na kumaliza tofauti kwa kufuata itifaki, katiba na maadili ndani ya chama.
Alisema kihistoria NCCR- Mageuzi kimetoka mbali na kiliwahi kugawanyika vikundi viwili cha NCCR-Mageuzi na NCCR- Mageuzi Asilia, iliyoongozwa na Prince Bagenda.
“Mbatia uandike kitabu cha NCCR. Historia ni somo na mapitio, misukosuko mingi chama hiki kimepitia, ukikiumiza chama cha siasa kinahitaji miongo miwili kukiimarisha,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, aligoma kujibu mapigo ya Mbowe na kusema kuwa pale si mahali muafaka pa kufanya hivyo.
“Sikuja hapa kujibu mapigo, bali katika sura tatu. Mimi ni mshiriki wa TSD, vyama vyenye wabunge nchini, nimekuja kama mshiriki wa Baraza la Taifa la Mashaurino ya Vyama vya Siasa vyote vilivyosajiliwa chini ya msajili, ambavyo hukutana mara kwa mara kubadilishana mawazo na ndiyo sehemu ya kijibu mapigo,” alisema Mangula.
Alisema hapo ni mahali pa kutoa pongezi kwa hatua iliyofikiwa na NCCR ya uchaguzi, kutokana na ukomavu waliouonyesha.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo wa dini pamoja na vyama vya siasa, akiwamo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, Profesa Lipumba, Dk. Willbrod Slaa, Rashid Mtuta, Moses Machali pamoja na wajumbe zaidi ya 260 waliofika katika uchaguzi huo wa nafasi za ngazi za taifa.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment
Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako