
KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amepuuza majigambo ya Chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania), kuwa kitakisambaratisha chama hicho kutokana na kuchukua wafuasi wengi. Akizungumza na MTANZANIA Jumapili juzi, Dk. Slaa, alikishangaa chama hicho na kusema kuwa hayo ni maoni yao, hivyo hawezi kuongea chochote na kwamba anawashangaa kwa kujiona wako sahihi kusema hivyo.
“Siwezi kusema chochote, kwani hayo ni maoni yao na nawashangaa kama wanajiona wako sahihi kusema hivyo,” alisema Dk. Slaa.
Kauli ya Dk. Slaa, imekuja siku chache baada ya ACT-Tanzania, kupatiwa usajili wa muda na mmoja wa viongozi wa chama hicho, kuliambia gazeti dada la hili (MTANZANIA Jumatano), kuwa chama hicho kitakuwa tishio kwa Chadema, kutokana na kuundwa na vigogo wanaotoka kwenye chama hicho na wengine ambao watakihama punde, baada ya kutolewa maamuzi dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao, Zitto Kabwe.
Taarifa za kupatiwa usajili chama hicho, zilithibitishwa pia na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Francis Mutungi, ambaye alisema tayari kina usajili wa muda.
Hatua ya ACT-Tanzania, ambacho kinadaiwa kuundwa na watu waliofukuzwa kutoka kwenye vyama vya upinzani, vikiwemo Chadema, CUF, na NCCR-Mageuzi, kusema kuwa kinatarajia kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika mwaka huu, unaongeza hofu kwa baadhi ya vyama vya siasa kuporwa baadhi ya nafasi za uwakilishi.
Kutokana na hilo, baadhi ya wadau wa siasa nchini, wanakitabiria kushika nafasi ya juu katika medali ya siasa kwa wafuasi wengi wenye nguvu, kujiunga ndani ya chama hicho hasa kutoka Chadema, kutokana na kuwa na mgogoro unaoendelea hivi sasa.
Mgogoro huo uliosababisha kufukuzwa unachama kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, akikimbilia Mahakamani kuomba zuio la kutojadiliwa na kikao cha kamati kuu kilichowavua uanachama wenzake.
Dk. Kitila, Zitto Kabwe na Samson Mwigamba, walituhumiwa na uongozi wa juu wa CHADEMA, kwa kuandaa waraka wa siri wenye lengo la kufanya mapinduzi ndani ya uongozi wa chama chao.
Na Mtanzania
No comments:
Post a Comment
Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako