- Yadai kauli yake kwa mawaziri mizigo ina ukakasi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimempinga Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, kutokana na hatua ya kuwatetea baadhi ya mawaziri mizigo waliorudishwa tena kwenye Baraza la Mawaziri, huku kikisema kauli yake ina ukakasi. Msimamo wa CCM umekuja siku chache, baada ya Balozi Sefue kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kuwatetea mawaziri mizigo kwa kile alichosema hawapaswi kulaumiwa kutokana na wakati mwingine kucheleweshewa fedha kwenye wizara zao.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipingana vikali na kauli ya Balozi Sefue.
Alisema si kila jambo la utendaji ndani ya Serikali, limekuwa likisababishwa na ukosefu wa fedha, bali huchangiwa na uzembe wa baadhi ya watumishi waliopewa dhamana ya kuongoza wizara.
Alisema kamwe CCM haitanyamaza kutetea maslahi ya Watanzania na muda wote itawachukulia hatua za kinidhamu mawaziri na watendaji wa Serikali, ambao wamekuwa wakikwamisha kasi ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.
“Majibu ya Balozi Sefue yanaleta ukakasi, si kila jambo ni ukosefu wa fedha ila ni uzembe wa waliopewa dhamana ya kuongoza hasa wizara au idara.
“Kwa mfano katika suala la uchapaji wa vitabu, kulikuwa na fedha za kutosha tena kutokana na chenji ya rada, lakini leo hii mtu anachapa kitabu hakifai kabisa na kuna makosa 72 halafu unataka tunyamaze kimya…hapa unabaini kuwa tatizo si fedha ila ni uzembe tu,” alisema Nape.
Alisema katika ziara yao walioifanya mikoa ya nyanda za juu kusini, walishuhudia matatizo mengi ambayo kwa namna moja au nyingine yamesababishwa na viongozi.
Alisema kilichobainika katika ziara hiyo, baadhi ya viongozi wa Serikali walikuwa hawatimizi majukumu yao ipasavyo, hali iliyowafanya kila wakati wananchi walalamike.
“CCM inapozungumza ina ushahidi wa kutosha ambao mwisho wa siku, umethibitishwa na wananchi wenyewe. Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo hakuwahi kwenda hata kutembelea ghala la Taifa la Mkoa wa Ruvuma.
“Haiingii akilini hata kidogo, kiongozi umepewa dhamana alafu unashindwa kutembelea maeneo ambayo yako chini ya wizara yako kwa miaka minne, alafu sisi tukae kimya,” alihoji Nape.
Mawaziri mizigo
Akizungumzia kurudishwa kwa mawaziri mizigo, alisema wamepewa fursa ya kurekebisha upungufu na kuwataka wasibweteke, bali wawatumikie wananchi.
“Katika msafara wa mamba na kenge wamo, ifahamike kuwa CCM hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha upungufu na hata kutotimiza wajibu wao vizuri.
“Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu, ni kuhujumu ilani ya uchaguzi ya CCM na hatutavumilia usaliti huo, kwani kukaa kimya itakuwa ni kujinyonga sisi wenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa kuona,” alisema.
Hata hivyo, aliwatahadharisha watendaji wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao, kwa kuwataka kujiondoa wenyewe ila kama wamekubali kupewa dhamana ni vema wakakubali kuhojiwa na chama na si vinginevyo.
“Kama safari za waziri fulani kwenda nje ni nyingi kuliko za kwenda kuwatembelea wananchi, tukisema yanakuwa maneno… kwa hali hii wewe kama hutaki kusemwa au kuhojiwa na chama ondoka mwenyewe. Ila kama unajijua umepewa dhamana, basi elewa ukienda kinyume chama kitakuhoji na kama hauko tayari nenda ukalime,” alisema.
“Muda tuliobakisha wa kutekeleza ilani ya uchaguzi ni mdogo, kwa sababu ziko ahadi tulizoahidi kwa wananchi hivyo upya wao usiwe chanzo cha kusahau kama yako mapungufu,” alisema Nape.
Januari 19, mwaka huu akitangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Balozi Sefue aliwatetea mawaziri hao na kusema hawakupaswa kulaumiwa kwa sababu wengine walishindwa kutimiza majukumu yao kutokana na ukosefu wa fedha.
Mawaziri ambao walilalamikiwa, ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu, Dk. William Mgimwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa.
na NORA DAMIAN NA BEATRICE MAGORI, mtanzania
No comments:
Post a Comment
Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako