Wednesday, 22 January 2014

Raza awang’akia wanaotaka atimuliwe uanachama CCM

Zanzibar. Mwakilishi wa Jimbo la Uzini (CCM), Mohamed Raza Dharamsi amesema hakuna kifungu wala mwongozo wowote wa CCM unaomzuia mwanachama kutotumia demokrasia ya kukosoa ikiwemo muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Raza alitoa msimamo katika majibu yake ya maandishi alipotakiwa kujieleza mbele ya kamati ya siasa ya jimbo na wilaya huko Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja hivi karibuni.
Alisema tuhuma namba moja hadi nane zilizotolewa zimejaa upotoshaji na chuki za mwandishi aliyetayarisha tuhuma hizo 16 kabla ya kujadiliwa na vikao vya siasa vya jimbo na wilaya.
“Hakuna kifungu wala mwongozo wowote wa chama unaozuia wanachama kukosoa na kutumia demorasia ya kutaka marekebisho ya katiba ya nchi yetu na sheria zake zinalinda haki ya kutoa maoni,” alisema Raza katika maandishi yake. Raza alisema kama kuna mtu katika chama anatafsiri ukosoaji ni kejeli au dharau ,hilo ni tatizo lake binafsi na wala si la chama au ukiukaji wa sheria za nchi.
Alisema kwamba kwa upande wake amesikitishwa sana kuwepo kwa watu wachache ndani ya CCM wanavyopenda kukitumia chama na vikao vyake halali kwa ajenda zao binafsi, badala ya kutumia muda huo kukijenga chama na kinyume chake hutengeneza mifarakano.
“Mimi si mgeni hapa Zanzibar, nimeona na ninashiriki katika shughuli mbalimbali pia naona chama chetu kinavyojenga misingi ya kidemokrasia na uwazi wa hali ya juu,” alieleza Raza katika maelezo yake ya jumla ya barua yake.
Alisema ameshangazwa na hatua anazochukuliwa yeye wakati Katibu Mkuu wa CCM Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana katika ziara zake za kila siku amekuwa akikosoa utendaji wa viongozi wa chama na serikali licha ya kufanya kwake hivyo wapo wasiofurahi ila anatimiza uwazi wa demokrasia ndani ya CCM.
Alisema kuwa wapo wanaotofautiana naye kimtazamo, jambo ambalo ni sahihi katika kufuata misingi ya demokrasia na kuonya si vyema kutumia vikao vya chama ili kuendeleza chuki dhidi yake kwa vile kitendo hicho kinaweza kubomoa badala ya kukijenga chama chao.
Raza anasisitiza kuwa mambo ambayo amekuwa akiyazungumza dhidi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar amekuwa akiyazungumza kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita akiwa hadharani na kwa maandishi na kwamba alichokifanya si kitu kipya.
“Mimi nimefanya kazi na vingunge wa siasa wa Muungano na Zanzibar, nimekuwa na kina Rais wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Hayati Mzee Rashid Kawawa, Mzee John Malecela na Hayati Dk Omar Ali Juma, sasa nafanyakazi na Balozi Seif Ali Idd na Rais wa Zanzibar,Dk Ali Mohamed Shein,” alisisitiza Raza.
Alisema kwa bahati mbaya sana kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa na kinyongo tokea aingie na kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini kutokana na kufanya mambo makubwa yaliowashinda wengine hasa katika sekta ya elimu, maji, huduma za jamii kwa kushirikiana na Serikali.
“Mkanda wa video unaochukuliwa kama ushahidi haieleweki kama uliangaliwa na kamati nzima au ulitazamwa na mtu mmoja kwa utashi wake,ameandika utitiri wa tuhuma na kudai zinanikabili bila ya kusadikika,” alieleza Raza.
Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili Mwakilishi huo ni kuhoji uhalali wa Rais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohamed Shein kuunda Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba na Bunge lake, kitendo ambacho kiinapoteza kodi za wananchi.
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako