Tuesday, 28 January 2014

Mbunge awezesha vikundi vya wanawake

Mbunge wa viti Maalum (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Betty Machangu, amewashauri wananchi na vikundi vya ujasiria mali vya kinamama na vijana mkoani humo kuhakikisha wanajiunga katika vikundi ili iwe rahisi kupata misaada ya kuinua vipato vyao kutoka serikalini na baadhi ya taasisi mbalimbali nchini.  Machangu aliyasema hayo juzi mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya kuhamasisha vikundi vya wajasiriamali na kutembelea vikundi vyote vilivyopo katika Wilaya ya Moshi Vijijini na kuvipatia fedha baadhi ya vikundi.

Hadi sasa vikundi kadhaa vya ujasiriamali vimepokea zaidi ya Shilingi milioni 30 kutoka kwa mbunge huyo kwa ajili ya kuendeleza miradi.
Machangu alisema umoja utakaojengwa na wana-Kilimanjaro ndiyo utasaidia katika kuongeza vipato.

“ Kilimanjaro ni mkoa ambao una wananchi wanaopenda maendeleo, hilo tulikubali na ndiyo maana tuna jivunia na kama tutaendelea kujituma ni lazima mkoa wetu utakuwa mfano wa mikoa mingine,” alisema Machangu. 

Machangu amekuwa akitoa misaada kwa vikundi vya wanawake na vijana kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya hifadhi ya mazingira na ujasiriamali.

Hata hivyo, katika ziara hiyo alikutana na changamoto mbalimbali zikiwamo za matatizo ya miundombimu ambayo yamekuwa kikwazo kwa maendeleo katika baadhi ya vijiji.
Mbunge huyo aliwaahidi wananchi hao kwamba atazifikisha kero hizo katika mkutano ujao wa Bunge. 
na KAMILI MMBANDO, NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako