
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amejisalimisha mikononi mwa polisi mkoani hapa baada ya kutakiwa kwenda kuandika maelezo ya uharibifu wa mali. Lema aliwasili kituoni hapo jana mchana akiongozana na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Efatha Nanyaro na viongozi wengine na kuelekea kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, OCD Gileas Mroto.
Akizungumza nje ya ofisi za polisi wilaya, Lema alisema alipigiwa simu na OCD Mroto akimuomba kufika kituoni hapo kwa ajili ya kuandika maelezo.
“Leo ndiyo nimejua kwamba ninatafutwa sikuwa na hizo taarifa … OCD amenipigia na kwa vile natambua yule ni kiongozi mwenzangu niliamua kwenda kumsikiliza,” alisema Lema na kuongeza:
“Polisi wameniambia ninawajibu wa kutoa maelezo ila tumekubaliana kwamba nirudi Jumanne Februari 11, mwaka huu kwani sikuwa tayari kutoa maelezo kwa sababu wakili wangu hayupo,” alisema.
Alisema baada ya kukubaliana hivyo polisi walimruhusu kuendelea na kampeni za chama chake katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Sombetini unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.
Lema alisema taarifa alizoambiwa ni kuwapo uharibifu wa gari mbili za Hiace wakati wa mkutano wa kampeni, alidai vurugu hizo zilisabishwa na CCM na CHADEMA.
“Nimeambiwa kulikuwa na Hiace mbili zinapita wakati vurugu za kurusha mawe, vurugu hizo zilifanywa na CCM kwani hata picha na video na mnato tunazo.
“Kabla ya Jumanne tutakuwa tumeziweka hewani hizo picha zote ili watu waone nani walikuwa wakifanya vurugu katika eneo hilo la Safina,” alisema Lema.
Vyama vya CCM na CHADEMA katika uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini Jimbo la Arusha vimekuwa vikituhumiana kufanyiana fujo huku kila Chama kikimrushia mwenzake kuhusika na vurugu.
NA ELIYA MBONEA, ARUSHA - mtanzania
No comments:
Post a Comment
Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako