Friday, 7 February 2014

Baregu aonya kuhusu Bunge Maalumu

8E9U6011
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu amesema, Bunge maalumu lijao la Katiba linaweza kugeuka kituko iwapo wajumbe wake wataweka mbele masilahi ya vyama vya kisiasa na kuacha misingi ya kujenga taifa moja na lenye mshikamano. Pia amesema, pamoja na Tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake lakini kwa upande mwingine hatakubali kukaa kimya pindi atakapoona kazi nzuri iliyofanywa ya ukusanyaji maoni ya wananchi ikidhihakiwa.
“Sitaweza kukaa kimya eti kwa sababu Tume imemaliza kazi yake huku nikiona watu wanapindisha mambo na kukebehi kazi nzuri ya Tume,” alisema.
Akizungumza kwenye kongamano lilipewa jina,“Katiba moja kwa Watanzania wote-Pamoja tutafika,” Prof Baregu alisema bila kuweka utashi wa kujenga taifa moja, Bunge lijalo linaweza kutawaliwa na vituko.

“Iwapo wajumbe watakwenda kwenye Bunge la Katiba huku wakiwa na ushabiki wa vyama vyao mimi naona kutakuwa na vituko vikubwa.Tunapaswa kutambua kwamba tunakwenda kutengeneza Katiba ya Taifa na siyo kwa kuegemea masilahi ya kundi fulani,” alisema.
Alisema itakuwa siyo jambo la busara kuona wajumbe wakielekea kwenye Bunge hilo huku wakiwa tayari wamevalia nguo rasmi za vyama vyao kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kutia doa mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Prof Baregu aliwataka wajumbe watakaokuwa kwenye Bunge lijalo kutumia lugha sahihi inayoeleweka kwa wananchi badala ya kuchanganya lugha kama inavyojitokeza sasa katika vikao mbalimbali vya Bunge.

Henzron Mwakagenda kutoka Jukwaa la Katiba alisema ufanisi wa bunge lijalo unatia mashaka.

“Sisi tulikuwa kwa kwanza kupinga suala la wabunge kuwa sehemu ya bunge hili na tulipinga pia Rais kuteua wajumbe. Inavyoonekana sasa Bunge hili lijalo huenda lisiwe na tija,tunakusudia kuandaa kongamano maalumu”.
Prof. Baregu atoa somo kwa wabunge
RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kuwashauri wabunge kuboresha rasimu ya pili ya Katiba inayokwenda kujadiliwa hivi karibuni katika Bunge la Katiba, mjini Dodoma badala ya kuijadili kwa masilahi ya vyama vyao.

Ushauri huo ulitolewa jijini Dar es Salaam jana na mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alipozungumza na waandishi wa habari katika kongamano la Katiba ambalo lilijumuisha watu kutoka asasi mbalimbali.

“Kuna kazi kubwa ya kuipitia rasimu hiyo na kuirekebisha na tuache mambo ya serikali mbili au tatu, kwani hiyo ni kupotosha maana nzima ya Katiba wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefanya kazi katika mazingira magumu,” alisema.
Aidha, alisema anatumaini Watanzania watafika mahali watazungumzia mambo muhimu ya nchi kuliko kuzungumzia mambo ya kutaka vyeo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Tanzania (TAPID), John Malya, alisema Katiba itakayojadiliwa iwe ni ya manufaa kwa Watanzania na yenye kuleta muafaka kwa taifa kwa ujumla.

Na George Njogopa, Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Tuandikie maoni yako kuhusu habari hii
Asante kwa Mchango wako